Parliament of Tanzania

WARAKA WA SPIKA NA. 6/2017 KUHUSU KUUNDWA KWA KAMATI MAALUM YA USHAURI KUHUSU SEKTA NDOGO YA GESI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

BUNGE LA TANZANIA

WARAKA WA SPIKA NA. 6/2017

KUHUSU

KUUNDWA KWA KAMATI MAALUM YA USHAURI KUHUSU NAMNA

YA KULIWEZESHA TAIFA KUNUFAIKA NA MAPATO YATOKANAYO

NA SEKTA NDOGO YA GESI

(Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016)

_________________________

17 NOVEMBA, 2017

WARAKA WA SPIKA NA. 6/2017

KUHUSU

KUUNDWA KWA KAMATI MAALUM YA USHAURI KUHUSU NAMNA

YA KULIWEZESHA TAIFA KUNUFAIKA NA MAPATO YATOKANAYO

NA SEKTA NDOGO YA GESI

(Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016)

_________________________

1. Waheshimiwa Wabunge, hivi karibuni, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria mbili mpya zinazohusu usimamizi wa rasilimali za taifa na kufanyia marekebisho Sheria ya Madini. Sheria hizo mpya ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti hasi (unconscionable terms) katika mikataba ya rasilimali za nchi, 2017 (The Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Re-negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017. Sheria hiyo inalipa Bunge mamlaka ya kupitia makubaliano yoyote yaliyoingiwa na Serikali yakihusisha rasilimali za nchi.

2. Waheshimiwa Wabunge, Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti hasi katika mikataba ya rasilimali za nchi, 2017 inatoa fursa kwa Bunge kushiriki katika kupima masharti ya mikataba na makubaliano mbalimbali yaliyowahi kuingiwa yakihusisha rasilimali za nchi na kutoa mapendekezo ya namna ya kuyaboresha kama itaonekana haja ya kufanya hivyo.

3. Waheshimiwa Wabunge, kwa nyakati tofauti yametolewa maoni mbalimbali kuhusu mapitio ya baadhi ya mikataba inayogusa rasilimali za taifa, ikiwemo gesi. Ugunduzi wa gesi nchini uliibua matumaini kwa wananchi kwamba rasilimali hiyo ingesaidia kuinua uchumi wa nchi na hali ya maisha ya wananchi. Hata hivyo, matumaini hayo yameanza kufifia.

4. Waheshimiwa Wabunge, Taarifa zilizowahi kuwasilishwa Bungeni zimebainisha changamoto na dosari zilizopo katika makubaliano ya uzalishaji wa pamoja na utekelezaji wake (Production Sharing Agreements) ambapo ilionekana kabisa kwamba makubaliano hayo hayana manufaa kwa Taifa. Mfano wa maeneo yenye dosari katika makubaliano hayo ni: -

(a) Utaratibu wa kuchangia gharama baina ya Serikali na mbia wake;

(b) Wabia kuwa na hisa za kipaumbele (Redeemed Preference Share) wakati Serikali ina hisa za kawaida;

(c) Uendeshaji wa Chombo cha Pamoja (Special Purpose Vehicle) ambapo Chombo hicho kinawaajiri wabia;

(d) Utaratibu wa kugawana gawio baina ya Serikali na mbia wake unaowapa wabia haki ya kupata gawio bila kujali faida inayopatikana na Serikali kupata gawio kutegemea faida itakayopatikana;

(e) Haki ya ushiriki wa wabia katika miradi inayotekelezwa (back-in-rights) kwa namna inayoinyima Serikali haki ya kushiriki katika uwekezaji;

(f) Ucheleweshaji wa tathmini na ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya mbia wa Serikali, jambo linaloathiri marekebisho ya dosari zinazobainika.

5. Waheshimiwa Wabunge, hali hiyo ni miongoni mwa sababu za Kamati ya Nishati na Madini kuunda Kamati Ndogo ya kushughulikia masuala ya Sekta Ndogo ya Gesi mwaka 2011. Aidha, Kamati hiyo imeendelea kutoa mapendekezo yaliyochukuliwa na Serikali kwa vipindi tofauti. Hata hivyo, bado changamoto hizo zimeendelea.

6. Waheshimiwa Wabunge, pamoja na jitihada hizi, bado kumekuwepo na ulazima wa Bunge kuchukua hatua za makusudi kushughulikia kwa kina masuala mbalimbali katika sekta hii.

7. Waheshimiwa Wabunge, kwa maelezo hayo, ipo haja kwa Bunge kufanya tathmini ya kina ya Sekta Ndogo ya Gesi ili kutoa mapendekezo kwa Serikali na ikibidi kushauri marekebisho katika mikataba na mifumo kwa lengo la kuwezesha Taifa kunufaika ipasavyo. Hivyo, kwa mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, nimeamua kuunda Kamati Maalum ya Ushauri kuhusu namna ya kuliwezesha Taifa kunufaika na sekta ndogo ya gesi.

8. Waheshimiwa Wabunge, Kamati hiyo itakayokuwa na wajumbe kumi na moja (11) itafanya kazi kwa muda wa siku thelathini kuanzia tarehe watakayojulishwa na Katibu wa Bunge na baada ya kukamilisha kazi yake itawasilisha taarifa kwangu ili taratibu zingine muhimu zifuate. Kamati hiyo itazingatia Hadidu za Rejea zifuatazo: -

(a) Kubainisha dosari za kisera na sheria na kisheria katika kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya uzalishaji wa pamoja na uendeshaji wa shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya gesi nchini;

(b) Kubainisha masharti hasi (Unconscionable terms) katika makubaliano na mikataba ya utafutaji na uchimbaji wa gesi nchini;

(c) Kupendekeza namna bora ya usimamizi na uendeshaji wa masuala ya gesi nchini;

(d) Kutoa mapendekezo kuhusu namna bora ya uingiaji wa mikataba ya uchimbaji, utafutaji na biashara ya gesi nchini; ; na

(e) Kushughulikia jambo jingine lolote linalohusiana na sekta ndogo ya gesi nchini.

9. Waheshimiwa Wabunge, ili kufanikisha kazi hii, nimewateua Wajumbe wafuatao kuunda Kamati hiyo: -

(i) Mhe. Innocent Lugha Bashungwa, Mb.

(ii) Mhe. Dustan Luka Kitandula, Mb.

(iii) Mhe. Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mb

(iv) Mhe. Wanu Hafidh Ameir, Mb.

(v) Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa, Mb.

(vi) Mhe. Ruth Hiyob Mollel, Mb.

(vii) Mhe. Richard Philip Mbogo, Mb.

(viii) Mhe. Omar Mohamed Kigua, Mb.

(ix) Mhe. Abdallah Ally Mtolea, Mb.

(x) Mhe. Sebastian Simon Kapufi, Mb.

(xi) Mhe. Doto M. Biteko, Mb - ambaye atakuwa Mwenyekiti

Uamuzi huu nautoa leo tarehe 17 Novemba, 2017

Mhe. Job Y. Ndugai, Mb.

SPIKA

17 Novemba, 2017


Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's