Parliament of Tanzania

Bunge la Tanzania lapokea mwaliko wa kujiunga na Umoja wa Mabunge ya Afrika

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepokea mwaliko wa kujiunga na Umoja wa Mabunge ya Afrika (African Parliamentary Union).

Mwaliko huo uliwasilishwa na Rais wa Umoja huo ambaye pia ni Spika wa Bunge la Guine-Bissau Mheshimiwa Cipriano Cassama.

Akipokea mwaliko huo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai alisema ameupokea mwaliko huo kwa mikono miwili na kwamba ataufanyia kazi.

Spika Ndugai amepokea mwaliko huo punde baada ya kurejea nchini hii leo ambapo alikuwa nje ya nchi kwa takribani mwezi mmoja akifanya ziara ya Kibunge katika nchi mbalimbali.

Awali Mheshimiwa Spika Ndugai alihudhuria katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika uliofanyika Mjini Abuja ambapo katika mkutano huo alichaguliwa Mwenyekiti wa Maspika na Viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika.

Kwa wadhifa huo, Mhe Ndugai ataongoza Maspika wenzake toka Mabunge na Mabaraza ya kutunga Sheria 63 yaliyoko katika nchi 18 za Jumuiya ya Madola kwenye Bara la Afrika.

Aidha mara baada ya Mkutano huo Spika Ndugai alitembelea Bunge la Umoja wa Falme za Kiarabu na kufanya mazungumzo na Spika mwenzake, Mhe Dr Amal Al Qubaisi ambapo aliwasilisha mapendekezo rasmi ya kuanzisha Urafiki wa Kibunge baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mbali na hayo Mhe Ndugai kwa niaba ya Maspika wa Afrika alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais wa 12 wa Iran ambapo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, Rais huapishwa Bungeni na Spika.

Baada ya hafla hiyo Mhe. Spika Job Ndugai alipata wasaa wa kukutana na Spika wa Bunge la Iran, Mhe. Dkt. Ali Larijani na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano ya kibunge baina ya Bunge la Tanzania na Iran

Kwa upande mwingine akiwa mjini Tehran, Iran Spika wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mpya wa Iran, Mheshimiwa Hassan Rouhani ambapo Mheshimiwa Spika alimpongeza kwa kuchaguliwa kwake kwa mara ya pili na kumuahidi ushirikiano wa karibu baina ya Bunge la Tanzania na lile la Iran.

Spika Ndugai amrejea nchini wakati baadhi ya Kamati za Bunge zimeshaanza kukutana huku nyingine zikitarajiwa pia kuanza kukutana kuanzia wiki ijayo kabla ya kuanza kwa mkutano nane wa Bunge ambao unatarajiwa kuanza Septemba 05, 2017.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's