Parliament of Tanzania

WARAKA WA SPIKA NA. 5/2017 KUHUSU KUUNDWA KWA KAMATI MAALUM YA USHAURI KUHUSU SEKTA YA UVUVI

WARAKA WA SPIKA NA. 5/2017

KUHUSU

KUUNDA KAMATI MAALUM ITAKAYOLIWEZESHA BUNGE KUISHAURI SERIKALI KUHUSU CHANGAMOTO ZINAZOSABABISHA SEKTA YA UVUVI KUTOCHANGIA PATO LA KUTOSHA KATIKA UCHUMI WA TAIFA

________________________

(Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016)

_________________________

1. Waheshimiwa Wabunge, Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea Fishing) ni moja eneo ambalo lina fursa ya kulipatia Taifa mapato makubwa sana kutokana na hazina ya ukanda wa bahari tulionao.

2. Waheshimiwa Wabunge, hii ni Sekta ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kwenye mapato ya Taifa ya nchi jirani hapa Afrika kama vile Mauritius, Namibia, Seychelles na Sierra Leone. Mfano, Namibia, uvuvi huu unachangia takariban 10% ya pato la Taifa wakati Tanzania Sekta hii inachangia 1.4% tu ya Pato la Taifa. Aidha, kiwango hicho kwa Tanzania ni kwa Uvuvi wa Maji Baridi na Bahari wakati hiyo 10% ya Namibia ni kwa Uvuvi wa Bahari Kuu peke yake.

Waheshimiwa Wabunge, ingawa Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 inataka samaki waliochakatwa ili kuuzwa nje ya nchi kulipiwa mrabaha, Sheria ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu haina kipengele hicho; na hivyo Serikali haipati mapato yatokanayo na mirabaha kwa meli zitakazopewa leseni.

Waheshimiwa Wabunge, bado kama taifa hatujatumia ipasavyo fursa za rasilimali zilizoko katika Bahari Kuu katika kujipatia mapato.

3. Waheshimiwa Wabunge, faida ya Uvuvi wa Bahari Kuu hutokana na mapato ya leseni za Uvuvi wa Bahari Kuu kwa meli za kigeni, viwanda vya mazao ya Uvuvi wa Bahari Kuu, ajira katika meli za uvuvi na viwanda hivyo. Aidha, nchi hupata fedha nyingi za kigeni kwa mapato ya Sekta hiyo.

4. Waheshimiwa Wabunge, ili kuhakikisha tunapata faida katika Sekta hiyo, Bunge lilitunga Sheria ya Bahari Kuu ya Mamlaka ya Usimamiaji wa Uvuvi wa Bahari Kuuu Na. 17 ya Mwaka 2007 (Deep Sea Fishing Authority Act. No. 17 of 2007) na baadaye kutoa kanuni za kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu mwaka 2009. Mamlaka hiyo ndiyo ilipewa jukumu la kuandaa na kusimamia Sera ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Mipango ya Sekta hiyo na masuala mengine.

5. Waheshimiwa Wabunge, hata hivyo, kama ilivyo kwa Sekta nzima, mamlaka hiyo ina changamoto za kimfumo na kiutendaji ambazo zinakwaza ufanisi wake hadi kufikia kuwa wategemezi wa takwimu zinazotolewa na wenye leseni ili wapate malipo badala ya wao kukagua na kutoa tozo kwa wenye leseni.

6. Waheshimiwa Wabunge, tatizo jingine linaloripotiwa sana katika Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu ni pamoja na kwamba Kanuni ya 10 ya Kanuni za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya 2009 inataka kiasi cha samaki walioidhinishwa kuvunwa kiandikwe katika leseni, jambo hilo halifanyiki na hivyo haijulikani na hivyo hatujui kiasi gani kinavunwa na tumebaki na makisio tu.

7. Waheshimiwa Wabunge, kwa takwimu za leseni za meli za uvuvi tunazozitoa na kwa kiwango cha Uvuvi wa Bahari Kuu katika nchi za majirani zetu, Taasisi za nje zinakisia kwamba Taifa linapoteza takriban Shilingi bilioni 400 au zaidi kwa mwaka. Hivi sasa tunapata Shilingi bilioni 3.2 tu kwa mwaka.

8. Waheshimiwa Wabunge, kwa kutambua umuhimu wa Sekta hiyo na pia faida tutakazoweza kupata kama Taifa, nimeamua kuunda Kamati Maalum ya Ushauri kwa mamlaka niliyopewa na Kanuni ya 5(i) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 inayonipa mamlaka ya kuweka utaratibu kwa jambo ambalo halijawekewa utaratibu au lililofanyiwa uamuzi awali na kuwa sehemu ya Kanuni za Bunge.

9. Waheshimiwa Wabunge, Kamati hiyo itakayokuwa na Wajumbe kumi na moja (11) itafanya kazi kwa muda wa siku thelathini (30) na baada ya kukamilisha kazi yake itawasilisha taarifa yake kwangu ili nione namna ya kuifanyia kazi.

10. Waheshimiwa Wabunge, Kamati hiyo itazingatia hadidu za rejea zifuatazo: -

(i) Kubainisha hazina ya mazao ya Bahari Kuu na mahitaji muhimu katika uvunaji wake;

(ii) Kutathmini mifumo iliyopo ya usimamizi na udhibiti wa shughuli za mazao ya Uvuvi wa Bahari Kuu;

(iii) Kubainisha mapungufu ya kisheria, kisera, kiutendaji na kimfumo yaliyopo katika Sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu;

(iv) Kubainisha manufaa na hasara ambao Taifa linapata kutokana na masharti ya leseni za Uvuvi wa Bahari Kuu na utekelezaji wake;

(v) Kushughulikia jambo jingine lolote linalohusu Uvuvi wa Bahari Kuu.

11. Ili kufanikisha kazi hii, nimewateua Wabunge wafuatao: -

(i) Mhe. Mussa Azzan Zungu, Mb.

(ii) Mhe. Salum Mwinyi Rehani, Mb.

(iii) Mhe. Masoud Abdallah Salim, Mb.

(iv) Mhe. Tauhida Gallos Nyimbo, Mb.

(v) Mhe. Mbaraka Kitwana Dau, Mb.

(vi) Mhe. Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mb.

(vii) Mhe. Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mb.

(viii) Mhe. Stanslaus Shing’oma Mabula, Mb.

(ix) Mhe. Mussa Bakari Mbarouk, Mb.

(x) Mhe. Cosato David Chumi, Mb.

(xi) Mhe. Anastazia Wambura, Mb. - CCM ambaye atakuwa Mwenyekiti

Uamuzi huu nautoa leo tarehe 17 Novemba, 2017

Mhe. Job Y. Ndugai, Mb.

SPIKA

17 Novemba, 2017

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's