Parliament of Tanzania

Kamati za kudumu za Bunge zaanza kukutana Mjini Dodoma

Kamati za Kudumu za Bunge zimeanza kukutana leo tarehe 12 Machi, 2018 Mjini Dodoma ili kutekeleza majukumu ya kibunge kabla ya Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 03 Aprili, 2018.

Kwa mujibu wa Ratiba ya Shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge waliwasili Mjini Dodoma Jumapili tarehe 11 Machi, 2018 tayari kwa ajili ya kuanza kwa vikao vya Kamati ambavyo vinatarajia kwisha 30 Machi, 2018.

Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (7) ujumbe wa Wabunge kwenye Kamati za Kudumu za Bunge ulikoma mwisho wa Mkutano wa Kumi wa Bunge. Kwa sababu hiyo, kabla ya kuanza kwa Shughuli za Kamati, Mheshimiwa Spika amefanya uteuzi mpya wa wajumbe wa Kamati za Bunge kwa kipindi cha nusu ya mwisho ya Bunge la Kumi na Moja. Baada ya uteuzi huo, shughuli zitakazotekelezwa na Kamati hizo ni pamoja na:-

UCHAGUZI WA WENYEVITI

Baada ya uteuzi wa Wajumbe wa Kamati za Bunge, kutakuwa na Uchaguzi wa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati zote za Bunge kwa Mujibu wa Kanuni ya 116(10) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.

KUPOKEA WASILISHO LA SERIKALI KUHUSU KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI

Katika kipindi hicho cha vikao vya Kamati za Bunge, Wabunge watapokea Wasilisho la Serikali kuhusu Mpango wa Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.

KUFANYA ZIARA ZA UKAGUZI WA MIRADI

Kamati zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi ya Maendeleo iliyotengewa fedha katika Bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016. Kamati zitakagua miradi ya uwekezaji liyotekelezwa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma. Aidha, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi mingine iliyotekelezwa na Serikali ili kulinganisha matokeo ya utekelezaji na thamani halisi ya fedha za Umma zilizotumika katika miradi hiyo.

KUFANYA UCHAMBUZI WA BAJETI

Katika vikao hivyo pia Kamati zitafanya uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti za Wizara inazozisimamia kwa Mwaka wa Fedha unaoishia 2017/2018 kwa ajili ya kufanya ulinganisho kuhusu makadirio ya matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.

KUFANYA UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA UWEKEZAJI

Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya uchambuzi wa Taarifa za Uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.

UCHAMBUZI WA SHERIA NDOGO

Kamati ya Sheria Ndogo itafanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi wa Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's